Ads 468x60px

Labels

Tuesday, April 10, 2012

TAMKO

UDOMASA




                                               

                                                                                                                               

University of Dodoma, Chimwaga Complex, P.O. Box 259,Udom, Cell +255 755 210310,
+ 255 713 004127, 0653331003, 0713 477180, Email: udomasa2011@gmail.com



MSIMAMO WA WANATAALUMA WA UDOM KUHUSU MAAMUZI YA BARAZA LA CHUO KIKUU CHA DODOMA KUKATAA KUPOKEA MAJIBU YA KAMATI YA RUFAA YA NIDHAMU YA WAFANYAKAZI



UTANGULIZI

Kumekuwepo na matukio ya kufukuzwa kazi wafanyakazi wa UDOM hasa wanataauluma kwa nyakati tofauti tofauti hasa mwishoni mwa 2011 na mwanzoni mwa 2012 kwa sababu mbalimbali zikiwepo za kinidhamu na nyingine. Matukio haya ya kufukuza kazi yamekuwa yakikiuka taratibu halali za kisheria (Sheria Na 6, 2004 ya Ajira na Mahusiano kazini) pamoja na sheria na kanuni nyingine za umma. Tafsiri pekee ambayo imekuwa ikihusishwa na matukio haya ya fukuzafukuza ni ulipizaji wa kisasi kwa wanataaluma kwa kuendesha mikutano endelevu mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kutimiziwa madai mbalimbali yaliyokwamishwa kwa muda mrefu tangu Chuo kianzishwe.



Baada ya wafanyakazi waliofukuzwa kutoridhika na uhalali wa wao kufukuzwa, baadhi yao waliamua kuchukua hatua za kukata rufaa kwenye vyombo husika vilivyoundwa kwa mujibu wa sheria ili waweze kupata haki zao. Kwa upande wa chuo Kikuu cha Dodoma, chombo pekee chenye mamlaka ya kupokea na kusikiliza rufaa ni KAMATI YA RUFAA YA NIDHAMU KWA WAFANYAKAZI (Staff Disciplinary Appeal Committee) kwa mujibu wa sheria inayoongoza chuo yaani “University of Dodoma Charter” kanuni 58 (1). Uundwaji wa kamati hii ya rufaa ulikamilika mwishoni mwa mwezi wa kumi (10) 2011 baada ya muda mrefu toka chuo kianze kutoundwa, na mnamo tarehe 14/12/2011 katika kikao cha Baraza la Chuo, kamati ilipewa baraka ianze kazi rasmi tarehe 15/12/2011 yaani kesho yake.



Punde tu baada ya kamati kuanza kazi, rufaa za wafanyakazi watano (5) waliofukuzwa na tayari walishapeleka rufaa zao sehemu husika zilianza kutafutiwa utaratibu wa kusikilizwa. Kamati hatimae ilipanga na ilifanikiwa kusikiliza rufaa hizo mnamo tarehe 10/02/2012. Kwa maelezo ya mdomo toka kwenye kamati, majibu ya rufaa yatatolewa  baada ya kufikishwa kwenye baraza la Chuo ambalo lilifanyika tarehe 30/03/2012 siku ya Ijumaa. Kamati ilitimiza wajibu wake wa kupeleka taarifa ya majibu ili yapewe baraka ndipo yaweze kutolewa kwa wahusika.



Kwa mshangao mkubwa na kwa masikitiko ya ajabu, Baraza la Chuo lilikataa kata kata kupokea taarifa ya kamati kwa madai kwamba Menejimenti ya Chuo haikujulishwa kwa maandishi siku ambayo rufaa ilisikilizwa na hivyo mchakato wote haukuwa sahihi. Mbaya zaidi, Baraza liliamuru kamati irudie kusikiliza rufaa hizo upya.



Sisi wanataaluma wa UDOM tunapenda kueleza yafuatayo:

1.      Madai ya kuwa Menejimjenti ya Chuo haikujulishwa siku ya kusikiliza rufaa na hivyo haikuwakilishwa hayana msingi na ni propaganda za kupindisha ukweli kwani ushahidi unaonesha menejimenti ya chuo iliwakilishwa na maafisa wa chuo wanaotambulika. Waliowakilisha menejimenti wakati wa usikilizaji wa rufaa ni 1. Bi Subira Sawasawa (DHRMA) yaani Mkurugenzi wa rasilimali watu na utawala; 2. Bwana John Kusaja (PAO), yaani Afisa tawala mwandamizi na 3. Bwana Melkiori Sanga (LO) yaani Afisa Sheria wa chuo. Hawa watu walitumwa na nani na kwa maslahi ya nani?

2.      Kitendo cha agenda kutoka kwenye kamati ya rufaa kutopokelewa na Baraza la Chuo inaleta tafsiri ya kuwa pengine kuna ushawishi wa makusudi ulifanywa na menejimenti ya chuo ili kukwamisha agenda husika kwa sababu inazozijua yenyewe.

3.      Kitendo cha Menejimenti ya Chuo kupeleka malalamiko yake kwenye Baraza kwamba haikutendewa haki ni kuvuruga utaratibu wa kisheria uliopo kihalali kwani Baraza la Chuo lilishakamilisha kazi yake ya kufukuza na halipaswi kwa namna yoyote ile kuingilia kati utaratibu wa rufaa kinyume na utaratibu. Kama Menejimenti inaona haikutendewa haki, kuna vyombo halali vilivyopo kisheria ambapo inaweza kupeleka malalamiko yake na ikatendewa haki mfano CMA.

4.      Ifahamike pia kuwa kitendo cha baraza la chuo kuzima hoja kwa makusudi kutoka kwenye kamati ya rufaa ni matumizi mabaya ya baraza ambalo ni chombo muhimu sana katika taasisi hii ya elimu ya juu kwani si kazi yake kufanya hivyo.  

5.      Uamuzi wa Baraza la Chuo kuagiza kamati irudie kusikiliza rufaa upya ni kupindisha sheria kwa makusudi kwa maslahi yasiyojulikana na kuwafanya watu wengi kujiuliza maswali kulikoni majibu kutotolewa kwa muda wote huu, kuna nini?



Msimamo na Hitaji la UDOMASA

Tunapenda watu wote na umma kwa ujumla ujue msimamo na dai letu kuhusiana na jambo husika kama ifuatavyo

1.      Pamoja na kufahamu fika kwamba wafanyakazi wengi walifukuzwa bila kufuatwa taratibu za kisheria, sisi wanataaluma wa UDOM, tumeonesha ustaarabu wa kuridhisha kwa kuwashauri wenzetu waliofukuzwa kufuata njia na taratibu za kisheria ya kudai haki zao kwenye vyombo vilivyoundwa kisheria kwa kukata rufaa badala ya kuingia kwenye mikutano au migomo. Ustaarabu wetu huu unapaswa kutambuliwa

2.      Hatuko tayari kuona rufaa inasikilizwa upya kwani kufanya hivyo ni kutengeneza mazingira na desturi (precedence) ya sheria kupindishwa pasipo na sababu yeyote na pia ni tishio kubwa sana kwa misingi ya upatikananji haki sio tu kwa waliokata rufaa sasa bali hata kwa wafanyakazi wengine waliobaki kwa siku za usoni.

3.      Hitaji letu kwa sasa ni moja na ni rahisi sana; majibu ya kamati ya rufaa yatolewe, kama kuna upande wowote haujaridhika iwe upande wa Mlalamikiwa (Menejimenti ya chuo) au Walalamikaji (wakata rufaa) ni vema ufuate taratibu zilizopo kupata haki kwani sheria ziko wazi sana kwa manufa ya wote.

4.      Tuko tayari kutetea msimamo wetu huu kwa njia zote tunazoweza.



Imetolewa na

.........................

Paul Loisulie

Mwenyekiti wa UDOMASA  

No comments:

Post a Comment